Jumatano 22 Oktoba 2025 - 07:11
Ikiwa Iran itavamiwa, tutauwasha moto wa jahanamu

Hawza/ Generali mkuu wa Sepah Pasdaran Muhammad Pakpour alielezea utayari kamili wa Iran kutoa jibu thabiti kwa aina yoyote ya uvamizi na kusisitiza: tutamuwashia adui jahanamu

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Qasim al-Araji, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq, amekutana na Meja Jenerali Pakpour, Kamanda Mkuu wa jeshi la mapinduzi Sepah Pasdaran.  

Katika mazungumzo yao, Qasim al-Araji alimuwasilishia salamu za Rais na Waziri Mkuu wa Iraq Jenerali Pakpour, na kusisitiza dhamira ya Iraq ya kutekeleza makubaliano ya usalama kati yao na Iran. Alisema kwa maneno kuwa: “Usalama wa Iran ni usalama wa Iraq”, na akapinga vikali kutumika ardhi ya Iraq kwa shughuli zozote dhidi ya Iran. Pia alitangaza kuundwa kwa kamati ya pamoja itakayosimamia utekelezaji wa makubaliano hayo ya usalama na kuzuia harakati zisizo halali.

Al-Araji pia alizungumzia makubaliano ya kusitishwa mapigano huko Ghaza, akionesha kutokuwa na imani dhidi ya utawala wa Kizayuni (Israel), na kusema kuna uwezekano mkubwa wa kuvunjwa makubaliano hayo. Alisisitiza kuwa umoja wa nchi za eneo hili ndilo jambo la msingi katika kudumisha amani na utulivu.
  
Kuhusu vita vya siku 12 vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, alisema kuwa; adui alitarajia wananchi wa Iran wangeiasi serikali yao, lakini taifa la Iran lilionesha mshikamano wa kitaifa na uaminifu kwa misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa upande wake, Meja Jenerali Pakpour aliukaribisha ujumbe wa Iraq na kusema kuwa mazungumzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa Iraq katika kipindi hiki. Alionya kuwa maadui wa ukanda huu nia yao ni kudhoofisha umoja wa ndani wa mataifa. Alifichua kuwa katika vita vya siku 12, utawala wa Kizayuni ulipanga kuwaua makamanda na kusababisha machafuko ili kuvuruga mshikamano wa kitaifa wa Iran, lakini kwa hekima ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi na umakini wa wananchi, njama hiyo ilishindwa.

Kamanda Mkuu wa Sepah alisisitiza uwezo wa Iran wa kujihami katika vita hivyo, akisema:  
“Adui alidhania kwamba uwezo wetu wa makombora ungepungua katika siku za mwanzo, lakini tulijibu kwa nguvu na kwa usahihi mkubwa na tukaharibu malengo yaliyokusudiwa.”  
Akaongeza kwamba Iran iko tayari kikamilifu kutoa majibu makali kwa uvamizi wowote ujao, na akaahidi: “Tutauwasha moto wa jahanamu dhidi ya adui.”

Meja Jenerali Pakpour pia aliishukuru Iraq kwa hatua zake za kudhibiti makundi ya upinzani wakati wa vita hivyo na akasisitiza haja ya kutekeleza kikamilifu makubaliano ya usalama pamoja na kuunda kamati ya ardhini kwa ajili ya kusimamia maeneo ya mipakani. Alieleza kuwa makundi hayo ni tishio kwa usalama wa nchi zote mbili na yanapaswa kudhibitiwa kwa ushirikiano wa pamoja.

Kwa upande wake, Qasim al-Araji alisisitiza tena dhamira ya Iraq ya kuzuia hatua yoyote dhidi ya usalama wa Iran kupitia ardhi yake, akisema:  
“Katika vita vya siku 12 hatukuruhusu makundi ya upinzani kuchukua hatua yoyote, na katika siku zijazo pia tutazuia kwa uthabiti.”

Mwisho wa mazungumzo hayo, pande zote mbili zilikubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na kutekeleza makubaliano ya pande mbili. Maafisa wa Iraq walithibitisha uaminifu wao wa kimaadili na kisiasa katika kutekeleza ahadi zao kwa Iran.

Mwisho wa taarifa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha